Asilimia kubwa ya dawa ambazo zilikuwa zikitumika kutibu magonjwa mbalimbali kwa binadamu zilikuwa zikifanya hivyo kwa ufanisi mkubwa mno ukilingaisha na hali halisi ya wakati huu.
Baadhi ya dawa ambazo zilikuwa zikiaminika na walio wengi, hivi sasa uwezo wake umepungua katika kuua vijidudu ambavyo vimekuwa chanzo cha magonjwa kwa binadamu.
Mpenzi msomaji, hali ya dawa kushindwa kuua vijidudu au kuwaua bacteria ambao husababisha magonjwa kwa binadamu hujulikana kama Usugu wa dawa au kwa lugha ya kitaalam ni Antimicrobial Resistance.
Hali hii ya baadhi ya dawa kushindwa kuua vimelea visababishavyo magonjwa kwa binadamu, imegeuka kuwa tatizo kubwa hapa kwetu Tanzania na Dunia nzima kwa ujumla.
Kutokana na tatizo hili kuwepo, Serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa za matibabu katika kuwagharimikia wananchi huduma za matibabu. Aidha, kwa mwananchi mmoja mmoja imekuwa ni kero kwani inapelekea gharama za matibabu kuongezeka. Pia kutokana na mwananchi kuhangaika kupata dawa itakayomsaidia, inapelekea tatizo au ugonjwa kuwa sugu na hivyo kukwamisha shughuli za maendeleo na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Mambo na shughuli mbalimbali za mwanadamu zimekua zikisababisha tatizo hili kuwepo katika jamii. Miongoni mwa mambo au shughuli zisababishazo hali ya Usugu wa Dawa ni pamoja na:-
Matumizi ya dawa za binadamu katika kukuzia mifugo. Mpenzi msomaji, katika ufugaji wa mifugo dawa za binadamu zimekuwa zikitumika kwa malengo tofauti tofauti ambapo ni makosa yanayofanyika kwa kufahamu au kwa kutokufahamu. Hali hii inapelekea mlaji wa mwisho kutumia dawa iliyopo katika zao la mifugo bila kufahamu na hivyo baadae kuufanya mwili wake kuizoea dawa husika hata kama hana tatizo la kiafya.
Manunuzi na matumizi holela ya dawa pasipo ushauri wa wataalamu. Miongoni mwa maamuzi ambayo mgonjwa huweza kuyafanya ni kuwahi katika duka la dawa na kununua aina ya dawa kulingana na ufahamu alionao pasipo kufanya vipimo vya maabara au kupata ushauri kutoka kwa mtu sahihi. Pengine utasema kuwa huwezi kupanga foleni kumuona daktari, huwezi kupanga foleni katika maabara ili uweze kupima na kufahamu tatizo ulilonalo, hii inakufanya ujiaminishe kuwa una ugonjwa fulani na hivyo dawa yake pia unaifahamu na kuamua kuwahi katika duka la dawa na kununua hitaji lako. Mpenzi msomaji, ni vyema kununua au kupata dawa na kuitumia kulingana na utambuzi wa kitaalamu wa tatizo lako na pia ushauri sahihi kutoka kwa wataalam wa afya.
Kutokufuata maelekezo sahihi ya namna bora ya kutumia dawa. Namna bora au sahihi ya kutumia dawa ni pamoja na kutumia kipimo/idadi sahihi ya dawa/vidonge ambavyo unapaswa kutumia kwa mara moja, dose, ambapo kama ni vidonge vya kumeza viwili (inategemeana na uzito/mg ya dawa) basi iwe ni vidonge viwili, kama ni kipimo cha mililita kumi (10mls) basi iwe ni hivyo na siyo kinyume chake . Pia dawa hutumika mara kadhaa ndani ya siku moja, frequency, mfano utaambiwa umeze vidonge au upate sindano mara tatu au mara mbili kila baada ya masaa kumi na mbili au ishirini na nne, yapaswa ifanyike au itumike hivyo. Utapaswa kutumia dawa kwa muda wa siku tano, saba au mwezi mmoja,basi itapaswa iwe hivyo. Ndugu msomaji, yawezekana katika matumizi ya dawa ikawa kwa kufahamu au kutokufahamu umewahi kukengeuka juu ya namna bora ya kuitumia dawa husika, basi ni fursa nyingine ya wewe kuweza kufahamu au kukumbuka ili uweze kusaidia katika kupambana na tatizo hili la usugu wa dawa.
Maendeleo katika Jamii na Taifa kwa ujumla hutegemeana na nguvu kazi ya kutosha pamoja na Afya imara. Tatizo la usugu wa dawa, siyo tatizo la Serikali au kikundi Fulani katika jamii zetu, bali ni tatizo ambalo kila mmoja wetu anayo nafasi ya kusaidia ili kuweza kulipunguza kama siyo kulimaliza kabisa.
Kwa umoja wetu ikiwa ni pamoja na uwepo na uwezo wa wataalamu wa afya tulionao nchini, tunaweza kuondokana na tatizo hili la usugu wa dawa na kuwa na uhakika wa magonjwa kutibika pindi dawa zinapotumika.