Monday, June 22, 2020

DAWA ZITUMIKAZO KWA WATOTO


Watoto ni moja kati ya makundi katika jamii ambalo linahitaji uangalizi wa kutosha ili kuweza kuwa na ukuaji mzuri katika maadili, kiafya na hata kielimu. Makundi mengine yenye kuhitaji uangalizi ni pamoja na Wazee na mama wajawazito.
Ili mtoto aweze kukua vizuri kiafya, moja na mambo ya msingi ambayo atahitaji ni pamoja na lishe, pamoja na kupata chanjo au tiba sahihi kulingana na tatizo husika la kiafya.
Kwa upande wa matibabu kwa kundi hili la watoto, siku zote kumekuwepo na uangalizi au tahadhari mbalimbali ambazo zinalenga kumlinda mtoto ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa aina ya dawa ambazo atatumia zitakuwa ni zenye uwezo wa kufanya kazi kwa urahisi bila ya kuathiri mifumo ya mwili kutokana na mifumo hiyo kutokuwa imara ukilinganisha na mtu mzima.
Aidha sambamba na matibabu, pia kuna bidhaaa ambazo hutumika kwa watoto mfano sabuni za kuogea, mafuta ya kupakaa pamoja na poda. Bidhaa hizi hutengenezwa kwa kuzingatia uwezo wa mwili wa mtoto katika kuvipokea na hatimaye kufanya kazi husika.
Mambo au vitu vya msingi ambavyo huzingatiwa katika uandaaji wa bidhaa hizi pamoja na dawa kwa watoto ni uwezo wa kinga ya mwili kwa mtoto, uwezo wa viungo vyake katika kuyeyusha au kumeng’enya, lakini pia bidhaa hizi huandaliwa kwa namna ambayo bidhaa zitakuwa rafiki kwa matumizi ya mtoto, mfano kuandaa dawa ambayo ladha yake haitakuwa mbaya au chungu.
Ndugu msomaji, nimeanza na utangulizi huo ili kukukumbusha baadhi ya vitu ambavyo tayari unavifahamu. Lakini katika jamii zetu mara kadhaa kumekuwepo na matumizi ya bidhaa mbalimbali za afya pasipo kuzingatia kuwa itamnufaisha vipi mtumiaji. Mfano mtoto mdogo anapoogeshwa kwa kutumia sabuni za unga au za  kuogea watu wenye umri mkubwa/watu wazima, mafuta ya kupakaa, dawa ambazo hazijaandaliwa kwa kundi la watoto.
Kutokana na sababu mbalimbali, kuna nyakati ambazo katika familia zetu tumekuwa tukiwapatia watoto dawa ambapo kwa namna moja au nyingine dawa hizo zimewasaidia au kutowasaidia kwa kadri ilivyopaswa.
Katika hili tunaweza kujifunza kwa kupitia mfano huu, dawa yenye umbile la kidonge ambayo unapaswa kumpatia mtoto. Ni kweli kwamba watoto wadogo hawawezi kumeza kidonge au vidonge kwa urahisi, na badala yake dawa nyingi za watoto zipo katika umbile la kimiminika au syrup. Kwa dawa yenye umbile la kidonge ili mtoto mdogo aweze kumeza au kutumia, itahitajika kidonge kichanganywe na maji kidogo ili kiweze kutawanyika/kuyeyuka na hatimaye mtoto aweze kutumia kwa urahisi.
Mfano wa vidonge hivi ambavyo vinahitaji kuchanganywa na maji ili mtoto aweze kutuia kwa urahisi ni pamoja na dawa aina ya mseto (kutibu Malaria), Dawa aina ya Amoxycillin vidonge (Kutibu magonjwa ambukizi mfano kikohozi) pamoja na dawa za kutibu kifua kikuu.
Dawa hizi katika uandaaji mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na ladha ya kidonge baada ya kuchanganya na maji ili mtoto aweze kuipenda dawa (Ladha nzuri), harufu yake haimkwamishi mtoto katika kuitumia, lakini pia katika kipimo au dozi huwa ni sahihi kulingana na kundi la watoto.
Mambo ambayo hujitokeza kwa kutokuzingatia matumizi ya aina ya dawa kwa kundi la watoto ni pamoja na kutompatia mtoto dozi sahihi ya dawa (Kuvunja kidonge na kumpatia mtoto ni vigumu kupata dozi sahihi), kusababisha mtoto kutoipenda dawa na hatimaye kupata usumbufu katika kumaliza dozi (kuvunja kidonge kunaweza kufanya dawa kuwa la ladha ya uchungu baada ya umbile lake kuharibiwa). Kwa kutokuzingatia mambo hayo pamoja na sababu nyingine, kunasababisha lengo la matibabu kutofikiwa na hatimaye kupoteza ubora wa dawa.
Ili mgonjwa kuweza kunufaika na matibabu ikiwa ni pamoja na watoto, ni vyema matumizi ya dawa pamoja na bidhaa za afya yakafanyika kulingana na rika/umri wa mtumiaji pamoja na  ushauri tunaopatiwa na wataalamu wetu.
Share: